Promote your business for free

THIS BLOG IS SPONSORED BY AFRICAN SOCIAL NETWORK ,THE SOCIALY NETWORK PAY ITS USER IN POINTS BASED JOIN NOW AND SEE HOW MUCH MONEY YOU CAN MAKE USING SOCIAL NETWORK. | FEEL FREE TO ADVERTISE ON WWW.BONGLOB.COM

Saturday, 20 March 2010

Mabango ya Kanisa la Kakobe yavunjwa

Waandishi Wetu

MZIMU wa Shirika la umeme nchini umeendelea kumwandama Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Bible Fellowship la Mwenge jijini Dar es Salaam, Zachary Kakobe baada ya mabango ya kanisa lake kuvunjwa, kupisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo mkubwa.

Kutokana na hali hiyo Askofu Kakobe atawajibika kuilipa serikali fidia ya ubomoaji huo, kwa kile kinachoelezwa kuwa alikaidi kuondoa mabango mbele ya kanisa hilo ili kuruhusu njia ya umeme kupita.

Wiki chache zilizopita, serikali ilipuuzia mbali malalamiko ya Kakobe ya kutaka njia hiyo ya msongo mkubwa wa umeme kupita mbele ya kanisa hilo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam, James Nyabakari alisema jana kwamba tayari wametoa baraka zote kwa Tanesco kufanya tathmini ya kuondoa mabango hayo ili Kanisa la Askofu Kakobe liwajibike kuzilipa.

Jana Mwananchi ilishuhudia mafundi wa Tanesco wakiyaondoa mabango hayo mawili yenye urefu unakadiriwa kufikia futi 40 na upana futi 20 chini ya ulinzi wa polisi.

“Tutatoa agizo kwa Kakobe kulipa fedha hizo baada ya Tanesco kumaliza kazi na kuleta gharama walizotumia,” alisema Nyabakari.

Awali baadhi ya waamini wa kanisa hilo walionyesha kutaka kutoa upinzani ili kuzuia zoezi hilo, lakini walishindwa baada ya kuona linasimamiwa na polisi.

Tanroads ilikuwa imetoa notisi ya siku saba kwa kanisa hilo kuyaondoa mabango hayo, tangu Machi 9, mwaka huu kwa sababu yalikuwa yamejengwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara.

Nyabakari alisema kwamba hadi jana siku 20 zilikuwa zimepita na Askofu Kakobe alionekana kukaidi amri hiyo.

Hata hivyo, Kakobe jana hakupatikana kuzungumzia hatua hiyo ya Tanesco huku ikielezwa kuwa hayupo ofisini na hata alipotafutwa kwa simu, simu yake iliita bila majibu.

Mradi huo ulizusha mgogoro mkubwa kati ya Tanesco na kanisa hilo mwishoni mwa mwaka jana baada ya Askofu Kakobe kudai kwamba njia hiyo ya umeme ni hatari kwa afya ya waumini wake pamoja na vifaa vya elektroniki wanavyotumia kanisani.

Ilibidi Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kuingilia kati kwa kuitisha mazungumzo ya pande zote na baada ya wataalamu kutathmini malalamiko hayo, walibaini kwamba, mradi hauna madhara kwa binadamu na mali.

Njia hiyo ya umeme wa kilovoti 132, inaanzia Ubungo hadi kituo kidogo cha kusambazia umeme kitakachojengwa Makumbusho, wilayani Kinondoni.

Mradi huo utakaogharimu Sh34 bilioni, ni kwa ajili ya kuondoa tatizo la umeme mdogo katika maeneo mengi ya wilaya ya Kinondoni.

Akizungumza na mwananchi katika eneo la tukio, Meneja wa Miradi wa Tanesco, Norbert Ntimba alisema mabango hayo yalikuwa yanazuia utekelezaji wa mradi huo.

Awali kulikuwa na mvutano mkali kati ya kanisa hilo na Tanesco na kusababisha ujenzi huo kukwama hadi muafaka ulipofikiwa kati ya Askofu Kakobe na serikali kupitia Wizara ua madini na Nishati.

Katika kipindi cha zaidi ya wiki mbili za mvutano huo waumini wa kanisa hilo walijitolea kulinda usiku na mchana eneo hilo ili kuzuia ujenzi wa njia hiyo ya umeme wakidai kuwa unatawaathiri na pia utahatibu miundombimu ya kanisani kwao.

Habari hii imeandikwa na Elizabeth Ernest, Ezekiel Kaponela na Joyce Shella.

No comments:

Post a Comment